Sheria huduma za habari kufanyiwa Marekebisho kulinda uhuru wa habari
Na Marco Maduhu,Dar es salaam
WAZIRI Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa,amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA) katika nyanja mbalimbali, ikiwamo na kufanya Marekebisho ya sheria za huduma za habari ili kulinda uhuru wa habari.
Amebainisha hayo leo Mei 21,2024 wakati akitoa hotuba alipokuwa Mgeni Ramsi kwenye Kongamano (JUMIKITA) na Miaka Mitatu ya Rais Samia Madarakani,lililoendana Sambamba na Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari,ambayo kitaifa yalifanyika Mei 3 Jijini Dodoma.
Amesema anaipongeza Jumuiya hiyo kwa kuwaunganisha Waandishi wa habari za Mitandaoni kuwa wamoja, na kuwasihi wale ambao hawajajiunga na JUMIKITA wajiunge haraka, ili wawe kitu kimoja na kupatikana kwa urahisi.
"Serikali ipo tayari kushirikiana na JUMIKITA,na wale ambao hawajajiunga waenda ili muwe kitu kimoja,na sisi tunapowahitaji tujue tunawapata wapi na kwa urahisi,"amesema Majaliwa.
Amesema katika kuendelea kutoa Uhuru wa habari na kuulinda, Serikali itaendelea kufanya mapitio na mrekebisho ya Sheria za huduma za habari ambazo siyo rafiki.
Aidha,amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Mitandao ya Kijamii,na hata nchi za jirani ikiwamo Kenya zimekuwa zikiifuatilia nchi ya Tanzania kila kukicha,kutokana na kazi kubwa ambayo inafanywa na waandishi wa habari kwa kuitangaza nchi yao.
Amewasihi waandishi wa habari kuendelea kuitangaza Serikali kwa mazuri ambayo imeyafanya,ikiwamo na Miradi ya Kimkakati ambayo inaendelea kutekelezwa, pamoja na kuandika habari ambazo hazina viashiria ya uvunjifu wa Amani.
Katika hatua nyingine amesema kutokana na Mitandao ya Kijamii kuwa na Mchango mkubwa wa kutoa ajira kwa vijana, kwamba Rais Samia ameweka Mkakati wa kujenga Jengo kubwa la TEHAMA Jijini Dodoma,ambapo vijana wote wenye ubunifu watapata nafasi ya kulitumia.
Waziri wa habari, Mawasiliano na Teknlojia ya habari,Nape Nnauye, amesema ndani ya Miaka Mitatu ya Rais Samia wamepiga hatua kubwa katika Uhuru wa habari na hata kuongoza kwa nchi za Afrika Mashariki.
Amesema wakataa pia na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzanja (TCRA) kufanya Mapitio ya Sheria na kanuni ambazo zilikazwa sana ili zilegezwe, pamoja na mapitio ya Kodi na Tozo za kusajiri blog na Online TV,kwamba kusiwepo na utozwaji wa Tozo kwanza, bali Mwandishi aanze kufanya kazi na ikifika kipindi flani ndipo aanze kulipa.
Mwenyekiti wa JUMIKITA Shaaban Matwebe, akizungumza kwenye Jukwaa hilo, amempongeza Rais Samia kwa kutoa uhuru wa habari ndani ya miaka yake Mitatu ya Utawala,huku akiomba Serikali kuwathamini pia Waandishi wa habari wa Mitandao, pamoja na kuwapatia Matangazo mbalimbali.
Amesema baadhi ya viongozi wenye Mamlaka wamekuwa hawawathamini Waandishi wa habari za Mitandaoni hasa wanapokuwa wakipiga Simu ili kubalance habari.
Pia, ameziomba Mamlaka mbalimbali za Serikali kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa Mitandaoni Kitaaluma, ili wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao wafanye kwa ufanisi mkubwa.
Naye Milard Ayo ameiomba Serikali kupitia TCRA kwamba kutokana na Mitandao ya Kijamii kutoa ajira kwa vijana wengi na wengine wanatoka Vyuoni hawana Mitaji, wapunguze Ada za kusajili Blog sababu Sh.Laki Tano ni kubwa waipunguze pamoja na faini Sh.milioni 5, ili kutoa fursa ya Kwa vijana kuendelea kujiajiri.





