SERIKALI YATANGAZA NEEMA KWA WAZALISHAJI HABARI MTANDAONI IKIPUNGUZA ADA ZA UENDESHAJI, YAAGIZA WANAHABARI KULIPWA STAHIKI ZAO | Extra Mile

Thursday, February 12, 2026

SERIKALI YATANGAZA NEEMA KWA WAZALISHAJI HABARI MTANDAONI IKIPUNGUZA ADA ZA UENDESHAJI, YAAGIZA WANAHABARI KULIPWA STAHIKI ZAO

  Extra Mile       Thursday, February 12, 2026










Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, akizungumza wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji unaoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)


Serikali imetangaza kupunguza kwa kiasi kikubwa ada za usajili kwa watoa maudhui mtandaoni, hatua inayolenga kuvutia wadau wengi kujiunga na mfumo rasmi, kuongeza ushindani na kuboresha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa umma.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Vyombo vya Utangazaji (Annual Broadcasters’ Conference – ABC) 2026, uliofanyika leo Jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma (Mwana FA) amesema gharama ya leseni ya utoaji maudhui mtandaoni imepunguzwa kutoka shilingi 500,000 hadi 50,000, huku ada ya watoa maudhui ikishuka kutoka 1,000,000 hadi 100,000 kwa mwaka.


Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wa habari na mawasiliano, na kusisitiza kuwa msimamo huo hautabadilika.



“Serikali inaamini kwa gharama hizi nafuu, watoa maudhui wengi wataingia kwenye mfumo rasmi na hivyo kuongeza ufanisi, ushindani na ufikishaji wa taarifa sahihi kwa jamii,” alisema Mwinjuma.



Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo aliagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kushirikiana na Bodi ya Ithibati kuhakikisha utoaji wa leseni za utangazaji unazingatia mikataba na maslahi ya wafanyakazi wa vyombo vya habari.


Alisema amepokea taarifa kuwa baadhi ya vyombo havijalipa wafanyakazi mishahara kwa zaidi ya miezi sita, na kuagiza mamlaka husika kufuatilia suala hilo na kuwasilisha mrejesho ndani ya wiki moja.



“Nina taarifa kwamba kuna vyombo havijalipa wafanyakazi wake kwa zaidi ya miezi sita. Hili siyo suala la siasa, nataka mrejesho ndani ya wiki moja,” alisisitiza.


Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Watangazaji Huru Tanzania (NIBA), Amos Ngosha, akiwasilisha maoni kwa niaba ya vyama vya utangazaji, aliomba serikali kupunguza tozo nyingi zinazokabili sekta hiyo.



Alieleza kuwa vyombo vya habari hulazimika kulipa zaidi ya tozo 19 kila mwaka, kila moja ikiwa na sheria yake, hali inayodhoofisha uwezo wa kifedha wa taasisi nyingi za habari na kusababisha baadhi kushindwa kuendelea na huduma au kufungiwa.



Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Bakari, amesema mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kutoa mafunzo kwa wanahabari 2,054 nchini kote mwaka 2025.



Aliongeza kuwa usikivu wa redio umefikia asilimia 85, huku usambazaji wa televisheni kupitia satelaiti ukifikia asilimia 100. Pia alibainisha kuwa hadi Desemba 2025 jumla ya leseni 770 za utangazaji zilikuwa zimetolewa.



Dkt. Bakari alisema TCRA pia ina mpango wa kuanza mfumo wa redio kidijitali ili kuendana na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya soko la mawasiliano na kuwa itaanza katika mikoa mitano ambayo ni Dar Es Salaam, Dodoma, Arusha, Mbeya na Mwanza.

Mkutano huo wa siku mbili, unaofanyika Februari 12 na 13, 2026, umewakutanisha viongozi na wadau wa sekta ya utangazaji kujadili namna ya kuimarisha na kupanua huduma za utangazaji nchini ukichagizwa na kaulimbiu isemayo "Matumizi ya Teknolojia katika kupanua na kuboresha huduma za Utangazaji vijijini"







Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, akizungumza wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji unaoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika Ukumbi wa New Generation jijini Dodoma. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog








































logoblog
Previous
« Prev Post