Viongozi wa serikali za vijiji na kata kutoka maeneo ya Ruziba na Bisibo wilayani Biharamulo wameeleza kuridhishwa na elimu ya matumizi sahihi ya umeme na nishati safi ya kupikia iliyotolewa na wataalamu wa TANESCO mkoa wa Kagera, wakisema imeongeza uelewa na kuimarisha ushirikiano kati ya shirika hilo na wananchi.
Elimu hiyo ni mwendelezo wa kampeni ya uhamasishaji iliyoanza Februari 11, 2026, inayolenga kuwajengea uwezo viongozi na wadau kuhusu usalama wa umeme, ukaguzi wa mifumo ya waya, matumizi sahihi ya vifaa vya umeme, pamoja na faida za kutumia majiko ya umeme kama sehemu ya jitihada za kulinda mazingira. Wadau walioshiriki pia walionesha hamu ya kupata majiko hayo hata kwa gharama nafuu ili kuunga mkono matumizi ya nishati safi.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kagera, Mhandisi Tawakal Rwahila, alisema kuna miradi mikubwa ya umeme inayotarajiwa kutekelezwa mkoani humo kufuatia mikakati iliyokubaliwa na viongozi wa nchi za Afrika Mashariki walipokutana Dar es Salaam kujadili namna ya kuondoa changamoto za upatikanaji wa nishati. Alisema miradi hiyo itasaidia kuongeza upatikanaji wa umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo ya vijijini.
Kwa upande wao, viongozi wa Ruziba akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji cha Rugondo na Diwani wa kata hiyo, Donard Samson, walisema hatua ya TANESCO kuwakutanisha na kuwapa elimu inaonesha uwajibikaji na inaongeza imani kwa wananchi juu ya utekelezaji wa miradi ya umeme katika taasisi za umma na makazi ya wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Bisibo Busota, Divaston John, kwa niaba ya wananchi, aliahidi kuwa jamii iko tayari kushirikiana kulinda miundombinu ya umeme na kutoa taarifa za vitendo vya uharibifu kupitia namba ya huduma kwa wateja 180 ili kuhakikisha huduma inaendelea kuwa salama na endelevu.
Aidha, viongozi wa utendaji wa vijiji na kata walipongeza TANESCO kwa kuanzisha mifumo ya mawasiliano ya moja kwa moja na wananchi, wakisema imekuwa msaada mkubwa pale changamoto zinapotokea kwani hupata msaada kwa haraka. Pia waliipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhimiza matumizi ya nishati safi ambayo inalinda mazingira na kuboresha afya za wananchi.
Elimu iliyotolewa ilihusisha mada mbalimbali ikiwemo miradi ya umeme vijijini, usalama wa matumizi ya nishati, makundi ya tozo za umeme kwa wateja, pamoja na wajibu wa jamii katika kulinda miundombinu ya umeme. Viongozi walisisitiza kuwa uelewa huo utasaidia kupunguza ajali za umeme na kuongeza matumizi sahihi ya nishati katika ngazi ya kaya na taasisi.





