
Wajumbe kutoka taasisi ya kikanda ya elimu ya juu, Inter-University Council for East Africa (IUCEA), wamepongeza juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kuimarisha mafunzo ya vitendo kwa vijana kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), wakisema ni mkakati sahihi wa kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana.
Ujumbe huo kutoka nchi nane za Afrika Mashariki ulitoa kauli hiyo walipotembelea Chuo cha VETA Kagera kilichopo Bukoba Vijijini mkoani Kagera, ambako walipata fursa ya kushuhudia uwekezaji wa miundombinu na mbinu za kisasa za kufundishia ujuzi wa kazi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi wa Mafunzo wa VETA, Dkt. Abdallah Ngodu, alisema serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kila mwaka vijana wasiopungua 120,000 wanahitimu mafunzo ya ufundi stadi ili kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi nchini.
Aliongeza kuwa mwaka uliopita pekee wahitimu 86,000 walimaliza mafunzo katika vyuo mbalimbali vya ufundi stadi, hatua inayoonyesha kasi ya ukuaji wa sekta hiyo. Kwa sasa kuna takribani vyuo 80 vinavyotoa mafunzo hayo huku vingine 65 vikiwa katika hatua tofauti za ujenzi, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuhakikisha kila wilaya inakuwa na angalau chuo kimoja cha ufundi stadi.



