CHANJO YA POLIO YAZINDULIWA RASMI USHETU, WATOTO 148,00 KUFIKIWA | Extra Mile

Wednesday, March 25, 2026

CHANJO YA POLIO YAZINDULIWA RASMI USHETU, WATOTO 148,00 KUFIKIWA

  Extra Mile       Wednesday, March 25, 2026

 



Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu imezindua rasmi kampeni ya chanjo ya Polio yenye lengo_ la kuwalinda watoto dhidi ya ugonjwa huo hatari, ambapo zaidi ya watoto 148,000 wenye umri chini ya miaka 10 wanatarajiwa kufikiwa katika zoezi hilo.


Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 24 Machi 2026 katika Shule ya Msingi Nyamilangano, ukiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Bi. Hadija Kabojela, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Bi. Kabojela amesema kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hususan ugonjwa wa Polio ambao unaathiri afya na ustawi wa watoto. Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa jamii kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha watoto wote wanaostahili wanapatiwa chanjo hiyo kwa wakati.


Amefafanua kuwa chanjo ya Polio ni salama, imehakikiwa kitaalamu, na hutolewa bila malipo yoyote, hivyo hakuna sababu kwa mzazi au mlezi kushindwa kumpeleka mtoto wake kupata huduma hiyo muhimu. Aidha, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao katika vituo vya kutolea huduma ya chanjo vilivyo karibu nao ili waweze kufikiwa kwa urahisi.


Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, zoezi la utoaji chanjo litaendelea siku ya kesho katika kata zote ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, ambapo timu za wataalamu wa afya zitawafikia watoto katika maeneo mbalimbali ikiwemo vituo vya afya, zahanati pamoja na maeneo ya mikusanyiko ya jamii.


Kampeni hiyo inatarajiwa kuhitimishwa rasmi siku ya Ijumaa tarehe 27 Machi 2026, huku juhudi zikielekezwa kuhakikisha kila mtoto anayelengwa anapatiwa chanjo hiyo.






logoblog
Previous
« Prev Post