MADAKTARI 30 WA KICHINA KUTOA HUDUMA ZA KITABIBU BURE MACHI 28 NA 29 | Extra Mile

Tuesday, March 24, 2026

MADAKTARI 30 WA KICHINA KUTOA HUDUMA ZA KITABIBU BURE MACHI 28 NA 29

  Extra Mile       Tuesday, March 24, 2026



DAR ES SALAAM: Madaktari 30 kutoka China wanatarajiwa kuendesha kambi maalum ya siku mbili ya kutoa huduma za afya bure kwa wananchi wa Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam. Kambi hiyo itafanyika katika Kituo cha Biashara cha EACLC mnamo Machi 28 na 29, 2026, ikiwa na lengo la kuwasaidia wananchi kupata uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali bila malipo.


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amesema madaktari hao watatoa huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari, magonjwa ya moyo, saratani, shinikizo la damu pamoja na matatizo ya viungo kama pua na masikio.

“Tunawaalika wananchi wote kujitokeza kwa wingi. Wazazi na walezi wahakikishe wanawaleta watoto wao ili waweze kupimwa na kupata matibabu bure,” amesema Msando.


Kwa upande wake, Afisa Uhusiano na Habari, Linda Mtui, amesema kuwa kambi hiyo haitatoa tu matibabu bali pia ushauri wa kitaalamu kuhusu afya, pamoja na huduma maalum kwa wanawake na watoto. Ameongeza kuwa Kituo cha Biashara cha EACLC hakilengi biashara pekee, bali pia kinajali afya na ustawi wa jamii inayokihudumia.

Kambi hiyo inatarajiwa kuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Ubungo na maeneo ya jirani katika kuboresha afya zao.
logoblog
Previous
« Prev Post