
Wanariadha wa Tanzania wameendelea kuonesha kiwango cha juu cha ushindani katika mashindano ya YAS Kili International Half Marathon 2026, wakidhihirisha ubora wao katika mbio za masafa marefu barani Afrika. Mashindano hayo ya kilomita 21, ambayo ni sehemu ya tamasha kubwa la kila mwaka la Kili International Marathon, yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha afya kupitia mazoezi pamoja na kukuza vipaji vya wanariadha wa ndani na nje ya nchi.
Katika matokeo ya mwaka huu, upande wa wanaume ulitawaliwa na Mtanzania Michael Geay aliyenyakua medali ya dhahabu baada ya kumaliza mbio kwa muda wa saa 1:04:10. Alifuatiwa kwa karibu na Josephat Joshua Gisumo aliyetumia saa 1:04:14, huku Mkenya James Kairiuki akishika nafasi ya tatu kwa muda wa saa 1:04:30. Kwa upande wa wanawake, Hamida Musa aliibuka kinara kwa upande wa Watanzania, akifuatiwa na Failuna Matanga, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Mkenya Veronika Wanjiku.
Akizungumzia ushindi wake, Geay amesema kuwa ushindani ulikuwa mkali sana, lakini alijivunia kupeperusha vyema bendera ya Tanzania. “Nimefurahi sana kushinda. Haikuwa rahisi, kwani kila mmoja alikuwa analenga medali ya dhahabu,” amesema Geay. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, aliwapongeza wanariadha hao kwa nidhamu, uzalendo na jitihada zao. Aidha, alisoma salamu za pongezi kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameahidi kuwa mgeni rasmi katika mashindano ya mwakani pamoja na kuongeza zawadi kwa washindi hadi kufikia shilingi milioni 100.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas, Pierre Canton Bacara, alisema ushindani wa mashindano hayo unaendelea kuongezeka kila mwaka, huku akisisitiza dhamira ya kampuni hiyo katika kuendeleza michezo, kuimarisha uhusiano na jamii pamoja na kulinda mazingira kupitia miradi ya upandaji miti zaidi ya 50,000 katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro.
Ameongeza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ya “Kila Kona, Kila Hatua Kasi zaidi” inalenga kuonesha jitihada za kusambaza huduma za mawasiliano ya 4G na 5G nchini kote. Pia alibainisha kuwa kampuni hiyo imeendelea kutambuliwa kimataifa kwa ubora wa mtandao wake.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliipongeza Yas kwa mchango wake katika maendeleo ya jamii, akieleza kuwa mashindano hayo yamekuwa chachu ya kukuza utalii, biashara na uchumi wa mkoa huo.
Maelfu ya washiriki na mashabiki walijitokeza kushiriki na kushuhudia mashindano hayo, huku wanariadha wa Tanzania wakionekana kutawala ushindi katika makundi mbalimbali—jambo lililozua hamasa kubwa kwa wananchi. Mashindano ya yas Kili International Marathon 2026 yameendelea kuthibitisha nafasi yake kama moja ya matukio makubwa ya michezo barani Afrika, yakichangia kukuza uzalendo, kuhamasisha utalii na kuimarisha hadhi ya Tanzania katika mbio za kimataifa za masafa marefu.



