OFISI YA DKT. KIKWETE YAFICHUA UPOTOSHAJI WA TAARIFA ZA UWEKEZAJI WA MTANDAONI | Icon Communications

Monday, June 15, 2026

OFISI YA DKT. KIKWETE YAFICHUA UPOTOSHAJI WA TAARIFA ZA UWEKEZAJI WA MTANDAONI

  Extra Mile       Monday, June 15, 2026


                                                  TAARIFA KWA UMMA


Ofisi ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, inapinga na kukanusha vikali taarifa ya uongo na upotoshaji inayosambaa mitandaoni, ikidai kuwa Dkt. Kikwete anahusishwa na mradi unaodaiwa kuwa wa uwekezaji unaowaahidi Watanzania kipato cha uhakika kupitia jukwaa la kifedha linalotumia teknolojia ya akili mnemba.


Taarifa hiyo inadai kuwa maelfu ya Watanzania tayari wamenufaika na mradi huo baada ya kuwekeza kiasi cha shilingi 653,000, huku wakiahidiwa kupata zaidi ya shilingi 9,200,000 kwa mwezi. Madai hayo si ya kweli hata kidogo.


Ofisi ya Rais Mstaafu inapenda kuweka wazi kwamba Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete hajawahi kushiriki, kuidhinisha, kutangaza, kuunga mkono, wala kuhusika kwa namna yoyote ile na mpango huo wa kifedha. Ofisi yake haijawahi kuruhusu matumizi ya jina, picha, au heshima yake kuhusishwa na mradi huo unaodaiwa, na haitajihusisha na shughuli za aina hiyo.


Wananchi wanashauriwa kupuuza taarifa hiyo ya uongo na kuwa makini dhidi ya miradi ya kitapeli na vitendo haramu vya aina hiyo. Mtu yeyote atakayekutana na taarifa kama hizo za upotoshaji anapaswa kuzichukulia kama habari za uongo, kuepuka kuzisambaza, kujisajili, au kutuma fedha kwa mtu au jukwaa lolote linalohusishwa nazo.


TAARIFA YA UONGO IPUUZWE.

logoblog
Previous
« Prev Post